Tuesday, 19 June 2012 21:35
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, juzi walizozana katika kile kinachoonekana kuwa ni kuwania madaraka katika Jimbo la Bunda mkoani Mara, katika uchaguzi mkuu 2015.
Sakata hilo lilitokea nje ya ukumbi wa Bunge mara baada ya kuahirishwa kwa kikao juzi usiku, ambapo Wassira alimfuata Bulaya na kumhoji kwamba kwanini alitoa maneno ya kuipinga bajeti ya Serikali.
Wassira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM) alimwambia Bulaya: “Mimi ndiye Mbunge wa Bunda, wewe huwezi kujifanya ndiye uliyetumwa na wananchi kuja kusema maneno ya uwongo hapa, eti unaipinga bajeti ya Serikali, ni nani aliyekutuma?”
Waziri huyo alikwenda mbali na kumwambia mbunge huyo kijana kwamba, “wewe tunakufahamu una pande mbili (upinzani na CCM) na kila siku unashirikiana na Halima Mdee (Kawe-Chadema), tunakujua kwamba uko CCM na Chadema.”